Na Albogast Benjamin
Mabao matatu ya Andy Carroll ndani ya dakika nane kwenye London derby West Ham United dhidi ya Arsenal yamefanya mchezo huo wa mapema kwenye ligi ya England umalizike kwa sare ya mabao matatu shukrani za pekee kwa beki wa Arsenal Laurent Koscielny aliyepachika bao la kichwa na kufanya matokeo yawe 3 - 3.
Arsenal ilikuwa na dalili ya kuondoka na ushindi mapema kufuatia mabao ya mapema kupitia kwa Ozil dakika ya 18 akimaliza kazi nzuri ya kijana Iwobi, Dakika ya 35 Iwobi alirahisha kazi kwa Sanchez aliyepiga bao la pili na kufanya ubao usomeke 2 - 0.
Dakika 2 kabla ya mapumziko mshambuliaji wa Westham Andy Carroll aliharibu mipango kwa mabao mawili ya haraka Dakika ya 44' na 45' na kufanya timu hizo ziende mapumziko kwa kutoshana nguvu ya mabao 2 - 2.
Ilimchukua dakika 6 tu za kipindi cha pili Andy Carrol kuandika bao la 3 dk 52 na kumfanya afikishe mabao matatu "hat trick" ndani ya dakika 8 akiiweka mbele timu yake kwa mabao 3 - 2. Bao la Koscienly dakika ya 70 limeipa Arsenal pointi 1 katika michezo miwili dhidi ya Westham baada ya mchezo wa kwanza kwenye uwanja wa Emirates kumalizika kwa Arsenal kupoteza.