TIMU ya soka Azam, imezidi kujiweka tayari na michuano ya kimataifa msimu huu baada ya mwishoni mwa wiki kumtuma kocha wake msaidizi Dennis Kitambi, kwenda nchini Shelisheli kwa ajili ya kuutazama mchezo wa Light Stars ya nchini humo dhidi ya Bidvest Wits ya Afrika Kusini katika michuano hiyo.
Azam, wanaoshiriki michuano ya Kombe la Shirikisho, wamemtuma Kitambi kwa ajili ya kuwasoma vyema wapinzani waop licha ya kuwa na baadhi ya DVD za michezo yao ya hivi karibuni.
Taarifa iliyowekwa kwenye mtandao wa Azam, inasema kuwa Kitambi amesharejea nchini kwa kazi hiyo maalum na wamefanikiwa kuwasoma wapinzani wao wote huku akidai kuwa Bidvest ilitumia zaidi kikosi cha wachezaji wengi vijana kwa kuwapumzisha baadhi ya wachezaji wa kikosi cha kwanza.
“Dhumuni letu kwenda kule tulikuwa tunataka kuwaona wapinzani wetu tutakaocheza nao katika raundi inayofuata, tulipokwenda kule tulikuwa tunajua ya kuwa tutakutana na Bidvest katika raundi ijayo kutokana na aina ya mpinzani waliokutana naye, lakini tulikuwa tunataka kuhakikisha tunawaona Light Stars namna wanavyocheza, kwani huwezi kujua lolote linaweza kutokea kwenye soka.
“Bidvest tulishawasoma kwenye mechi zao nyingi za Ligi Kuu Afrika Kusini na tunazo baadhi ya DVD zao, lakini tulichokiona kule ni wao walitumia kikosi cha vijana zaidi na ni tofauti na tulivyowaona katika mechi zao za ligi,” alisema Kitambi.
Kitambi alisema kwa sasa wanachoangalia zaidi ni kusafiri tena kuelekea Afrika Kusini kuwasoma tena Bidvest Wits katika moja ya mechi yao ligi, ili kuwasoma zaidi wapinzani wao hao wanaofundishwa na Gavin Hunt.
Azam FC imejiweka malengo msimu huu kwenye michuano hiyo, ambapo imepanga kufika hatua ya robo fainali (hatua ya makundi) na ndio maana imesajili kikosi bora, imefanya maandalizi ya kutosha, kuboresha mfumo mzima wa kiuongozi pamoja na benchi la ufundi na kuwa wa kisasa zaidi.
Kwa mujibu wa droo ya michuano hiyo, Azam FC ndio timu pekee ya Afrika Mashariki iliyoanzia raundi ya kwanza, ambapo itaanzia ugenini kucheza mchezo wake wa kwanza dhidi ya moja ya timu hizo kati ya Machi 11, 12 na 13 kabla ya kumalizia nyumbani kati ya Machi 18, 19 na 20.