
KIPA WA SIMBA ATAMANI HAYA KATIKA TIMU YAKE KWA MSIMU HUU

KIPA namba moja wa Simba, Vicent Angban amesema anatamani timu yake iongoze msimamo wa Ligi Kuu bara baada ya mechi za mwishoni mwa wiki hii.
Simba inatarajiwa kucheza na Stand United kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa keshokutwa katika uwanja wa Kambarage, Shinyanga na endapo itashinda itaongoza msimamo wa kufikisha pointi 45 juu ya Yanga na Azam ambazo zina viporo.
Mara ya mwisho Simba kuongoza ligi ilikuwa ni mwanzoni mwa msimu wa mwaka 2013/14 ikiwa chini ya makocha wazawa Abdallah Kibadeni na Jamhuri Kihwelo, ‘Julio’ ambao waliiongoza timu hiyo kushinda michezo mitano mfululizo ya mwanzo mwa msimu.
kipa huyo raia wa Ivory Coast, Angban amesema atafurahi kuona timu yake inashinda mchezo wa Stand United na kuongoza kwenye msimamo wa ligi.
“Ligi ni ngumu na kila timu inataka kushinda lakini na sisi tunajitahidi kuona tunashinda kila mchezo kwani tunataka tuwe bingwa na kila mtu anawaza ubingwa tu,” alisema Angban.
Msimu wa mwaka 2014/15, Simba haikubahatika kufika nafasi ya pili katika msimu mzima hata kwa saa tu na badala yake walimaliza msimu wakiwa nafasi ya tatu.
Mara ya mwisho Simba kutwaa ubingwa ni msimu wa mwaka 2011/12, jambo ambalo mashabiki wana hamu ya kuona timu yao ikitwaa ubingwa kuepuka kuitwa wa mchangani na watani zao, Yanga.
Mechi ya Simba na Stand inatabiriwa kuwa ngumu kutokana na timu hiyo kuisumbua Simba msimu uliopita ambapo katika mechi ya kwanza zilitoka sare ya bao 1-1 kabla ya United kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mechi ya marudiano kwenye uwanja wa Kambarage.
Mechi ya kwanza msimu huu ilimalizika kwa Simba kushinda bao 1-0 katika Uwanja wa Taifa mechi ambayo Stand ilitawala karibu muda wote wa kipindi cha pili.