Our Feeds

Saturday, 13 February 2016

Unknown

YANGA KUPAA NA NYOTA HAWA 24 LEO

BAADA ya Yanga kukwama kuondoka juzi, wanatarajia kuondoka leo kwa ndege ya ATC kuwafuata Cercle de Joachim tayari kwa mchezo wa Jumamosi wa klabu bingwa Afrika utakaochezwa mjini Curepipe, Mauritius huku kocha mkuu wa Yanga Hans van Pluijm akisema wako tayari kwa mapambano.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga Jerry Muro, kikosi kitakachoondoka sio 21 na sasa hata wale waliopangwa kuachwa yaani Antony Mateo, Geofrey Mwashiuya na Benedikti Tinoco watakwenda na kufanya idadi ya wachezaji jumla kufikia 24.muroAwali, walitangaza kuondoka juzi kwa ndege ya Shirika la Ndege ya Afrika Kusini lakini ilishindikana baada ya shirika hilo kushindwa kuwapatia ndege ya kuunganisha mapema mjini Johannesburg kwenda Curepipe na hivyo wakaamua kukodi ndege ambayo itawasubiri baada ya mechi kesho na kuwarudisha.

“Safari imeiva, jumla ya wachezaji 24 wataondoka kuelekea Mauritius wakiongozana na viongozi saba wa benchi la ufundi, kikosi kimekamilika tunaomba mashabiki waiombee timu ifanye vizuri,” alisema Muro.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Jumamosi kuanzia Saa 9:30 alasiri kwa saa za Mauritius Uwanja wa Curepipe kabla ya timu hizo kurudiana wiki mbili baadaye Dar es Salaam. Kikosi hicho jana kilifanya mazoezi ya mwisho kwenye uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini.

Lengo la kwanza lililowekwa na timu hiyo ni kufika katika hatua ya makundi. Kocha wa Yanga Pluijm alisema kikosi kimejipanga na kiko tayari kwa mapambano.

Alisema mbinu atakazotumia hazina tofauti na zile ambazo amekuwa akitumia kwenye Ligi Kuu Tanzania bara.

Mkuu wa Msafara wa Yanga katika safari hiyo ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Ayoub Nyenzi wakati upande wa viongozi wa timu hiyo wanaokwenda ni Kaimu Katibu Mkuu, Baraka Deusdedit na Muro.

Kikosi kitakachoondoka leo ni Makipa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Deo Munishi ‘Dida’ na Benedicto Tinocco.

Washambuliaji ni; Malimi Busungu, Paul Nonga, Amissi Tambwe (Burundi) na Donald Ngoma (Zimbabwe).

Mabeki; Juma Abdul, Mbuyu Twite (DRC), Oscar Joshua, Mwinyi Mngwali, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Vincent Bossou (Togo) na Pato Ngonyani huku Viungo ni; Said Juma ‘Makapu’, Salum Telela, Thabani Kamusoko (Zimbabwe), Haruna Niyonzima (Rwanda), Simon Msuva, Issoufou Boubacar (Niger), Godfrey Mwashiuya na Deus Kaseke.

Kikosi hicho kitakaporejea kitakwenda moja kwa moja kuweka kambi Pemba kujiandaa na mchezo wa ligi dhidi ya watani wao Simba utakaochezwa Februari 20, mwaka huu.

Subscribe to Mtembezi Sports via Email :
Previous
Next Post »