Na Albogast Benjamin
Mahitaji ya wapenda soka wote nchini ni kuona timu zao zinafanya vizuri kimataifa na ikiwezekana kufika hatua za juu zaidi, na kama uwekezaji utaruhusu zaidi basi zifike zilipofika Tp Mazembe na Al Merreikh kwa timu zinazotoka upande wa Afrika mashariki na kati.
Kutokana na mipango mizuri iliyopo kwenye klabu ya Azam hakika si kitu kigeni kuona inaanza kuzifunga timu vigogo barani Afrika kama Esparance Sportive De Tunis iliyoanzishwa mwaka 1919 na imetwaa kombe hili zaidi ya mara moja pamoja na lile la ligi ya mabingwa.
Hili ndio darasa huru kwa soka la Tanzania ambalo mtembezisports iliwahi kuandika na kama wataendelea na mwenendo huu kwa kutumia benchi lao la ufundi pamoja na huduma zinazopatikana kwenye klabu watakuwa na nafasi nzuri ya kufika pale zilipokwama Yanga na Simba kisha wao ndo watasaidia kubadili mifumo ya vilabu hivi ambavyo kuzifunga timu kongwe za Afrika japo kwa mkondo wa kwanza imekuwa ni ndoto isiyo na mwisho.
Mchezo wa leo ulianza kwa timu zote kucheza kwa kusomana lakini makosa kidogo ya walinzi wa Azam kushindwa kujipanga na kumkabili vizuri mshambuliaji Jouin kutokana na urefu wake aliweza kuipa bao la kuongoza timu yake ya Esparance dakika 34 na likadumu kipindi chote cha kwanza.
Kipindi cha pili Azam waliongeza nguvu na wakashambulia kwa kasi kwa kutumia mipira ya chini na wakatumia vizuri nafasi kutokana na Esparance kuamini lengo lao la kupata ushindi au sare linakaribia kutimia ndipo Farid Musa akasawazisha dakika ya 68 kabala ya Ramadhani Singano kupachika bao la kuongoza dakika ya 69. Matokeo dakika 90 yakabaki 2 kwa Azam na 1 kwa Esparance.